Kituo cha Usalama na Faragha

Kuelewa mapendekezo kwenye Spotify

Je, mapendekezo ya Spotify hufanya kazi vipi?

Katika Spotify, tunalenga kutengeneza hali bora na za kipekee kwa kila mtumiaji. Lengo letu ni kumuunganisha kila mtu na kile anachopenda na kumsaidia kugundua kitu kipya. Hamna wasikilizaji wawili wanaofanana, hivyo hali ya matumizi ya Spotify ya kila mtu, na mapendekezo yetu mengi, huwekewa mapendeleo. Wanapoulizwa wanapenda nini kuhusu Spotify, wasikilizaji wengi hutaja mapendeleo tunayowawekea kama kipengele wanachopenda zaidi. Huenda ukajiuliza jinsi tunavyozalisha mapendekezo haya katika mipasho ya Mwanzo, orodha za kucheza, matokeo ya utafutaji au sehemu nyingine za huduma, na tungependa kubainisha jinsi yanavyofanya kazi.

Katika Spotify, watu na teknolojia hufanya kazi pamoja ili kuzalisha mapendekezo yanayofaa. Baadhi ya mapendekezo yanatokana na uratibu wa wahariri, kama vile orodha ya kucheza ya muziki wa pop iliyotengenezwa na waratibu wa muziki. Mapendekezo mengine huwekewa mapendeleo kulingana na hulka za kimuziki za kipekee za kila msikilizaji, kama vile orodha ya kucheza iliyowekewa mapendeleo inayoratibiwa na algoriti zetu zilizoundwa kitaalamu.

Tunaamini kuwa mapendekezo hayapaswi tu kuboreshwa ili kupata mbofyo unaofuata, bali kuendana na hulka yako kimuziki. Tuna timu zilizojikita katika kuhakikisha mapendekezo yako yanapelekea matumizi ya kweli na kukuza mitangusano inayofaa. Tunafanya kazi kuboresha mifumo yetu ya mapendekezo ili kuhakikisha tunakuonyesha maudhui yanayofaa na yanayofurahisha.

Uratibu unaofanywa na waratibu

Waratibu katika Spotify hutumia maarifa ya data, usikivu makini na uelewa wa mitindo ya kitadamuni ili kuweka maudhui pale ambapo yana uwezekano mkubwa wa kupendwa na mashabiki wengi zaidi ulimwenguni kote. Wanatumia uratibu makini kupendekeza maudhui kwenye Spotify, kama vile katika orodha za kucheza zilizoratibiwa. Ulimwenguni kote, waratibu katika Spotify wana maarifa mapana kuhusu muziki na utamaduni wa eneo husika, yanayowaruhusu kufanya maamuzi wa kuratibu muziki kwa kuzingatia hali bora zaidi za wasikilizaji.

Mapendekezo yanayokufaa

Spotify hutoa mapendekezo ya algoriti yanayofaa, ya kipekee na yaliyo mahususi kwa kila mtumiaji. Algoriti zetu huchagua na kupanga maudhui katika hali mbalimbali za Spotify za msikilizaji, ikiwa ni pamoja na Utafutaji, Mwanzo na orodha za kucheza zilizowekewa mapendeleo.

Ili kufanya mapendekezo haya, algoriti zetu hutegemea idadi fulani ya data. Umuhimu wa data hii unaweza kutofautiana katika kipindi cha muda, kulingana na matumizi yako ya Spotify. Tunaamini kuwa hulka yako kimuziki ndiyo kigezo muhimu zaidi kwa kukutengenezea hali bora zaidi ya matumizi kwa ujumla. Hapa chini, utapata maelezo zaidi kuhusu data muhimu zaidi na jinsi zinavyofanya kazi.

"Hulka yako kimuziki"

Unapotumia Spotify, vitendo kama vile utafutaji, usikilizaji, kuruka au kuhifadhi kwenye Maktaba Yako huathiri tafsiri yetu ya hulka yako kimuziki. Tunaita hali hii "hulka yako kimuziki," na huzipa algoriti zetu ishara ya yale yanayokuvutia na jinsi unavyopenda kusikiliza.

  • Mfano: Ikiwa unasikiliza msanii fulani, huenda tukapendekeza nyimbo zaidi za msanii huyo.
  • Mfano: Orodha yetu ya kucheza ya Release Radar hupendekeza matoleo mapya ambayo tunaamini utayafurahia kulingana na muziki unaofanana ambao ulisikiliza.
  • Mfano: Ikiwa unasikiliza podikasti ya michezo, huenda tukakupendekezea podikasti nyingine za michezo.

Maelezo unayoshiriki nasi

Mapendekezo hutokana pia na maelezo unayoshiriki na Spotify, kama vile mahali ulipo kwa jumla (si mahususi), lugha yako, umri wako na unaowafuatilia. Maelezo haya huzipa algoriti zetu ishara ya mada zinazokuvutia au wasanii ambao ungependa kupata taarifa zao.

  • Mfano: Iwapo unafuatilia podikasti fulani, huenda tukakupendekezea kipindi kutoka kwenye podikasti hiyo.
  • Mfano: Ukichagua Kijerumani kama lugha yako kwenye Spotify, huenda tukakupendekezea podikasti za lugha ya Kijerumani.

Maelezo kuhusu maudhui

Algoriti zetu huzingatia sifa za maudhui yenyewe, kama vile aina, tarehe ya kutolewa, aina ya podikasti, nk. Hatua hii huturuhusu kutambua maudhui gani yana sifa zinazofanana na yanayoweza kuwapendeza wasikilizaji wanaofanana.

  • Mfano: Iwapo unasikiliza muziki wa pop sana, huenda tukapendekeza nyimbo nyingine za pop zinazofanana.
  • Mfano: iwapo unasikiliza sana vitabu vya kusikiliza vya uhalifu, huenda tukapendekeza vitabu vingine vya kusikiliza vya uhalifu.

Usalama wa wasikilizaji

Kama mfumo, tunatathmini athari tuliyonayo kwa watayarishi, wasikilizaji na jumuiya. Spotify hufanya kazi kuhakikisha taratibu na michakato inayofaa ya usalama imewekwa, ikiwa ni pamoja na taratibu za kuzuia kuonyeshwa kwa maudhui hatari. Tunachukulia dhima ya algoriti kwa umakini na tunashirikiana kati ya timu za sera, bidhaa na utafiti, pamoja na kushauriana na wataalamu wa nje kama vile Baraza la Ushauri wa Usalama la Spotify.

Kanuni za Mfumo wa Spotify hutumika kwenye maudhui yote kwenye mfumo, ikiwa ni pamoja na maudhui yanayopendekezwa. Kanuni hizi zilitungwa na timu za ndani kwa kushirikiana na wataalamu wengi tofauti wa nje. Tunapofahamu kuhusu maudhui ambayo huenda yanakiuka kanuni, maudhui hayo hukaguliwa kulingana na sera zetu, na hatua inayofaa huchukuliwa. Hatua hizi ni pamoja na, kwa mfano, kuzuia maudhui yanayokiuka yasijumuishwe kwenye mapendekezo.

Je, unaweza kuathiri vipi vigezo ambavyo mapendekezo yako yanategemea?

Mapendekezo yako yanaathiriwa kila wakati na matumizi yako ya maudhui kwenye Spotify. Kadri unavyosikiliza zaidi maudhui unayopenda na kutumia zaidi programu, ndivyo tunavyoamini utafurahia zaidi mapendekezo yako.

Tunakupa pia njia za kuathiri na kutoa maoni kuhusu kinachoonyeshwa katika mapendekezo yako na kuonyeshwa maudhui machache zaidi ya kitu mahususi. Baadhi ya mifano imeorodheshwa hapa chini:

  • Usijumuishe kwenye hulka kimuziki: Unapochagua kutojumuisha orodha ya kucheza kwenye hulka yako kimuziki, orodha hiyo ya kucheza itakuwa na athari ndogo kwenye mapendekezo yako ya siku zijazo.
  • Kutoa maoni kuhusu mapendekezo: Unapogusa [sivutiwi/si bomba] kwenye mapendekezo katika Spotify, utapewa mapendekezo machache zaidi yanayofanana nayo.
  • Kichujio cha maudhui dhahiri: Unapozima maudhui dhahiri, chochote chenye lebo ya maudhui dhahiri kitazuiwa na hutaweza kukicheza.

Katika hali fulani, unaweza pia kupanga na kuchuja mapendekezo yako kulingana na unachotaka kuona zaidi. Kwa mfano, unaweza kuchuja ukurasa wako wa Mwanzo ili uone podikasti pekee, au uone muziki pekee.

Je, maamuzi ya kibishara huathiri vipi mapendekezo?

Spotify hutanguliza kuridhika kwa wasikilizaji wakati wa kupendekeza maudhui. Katika hali fulani, maamuzi ya kibiashara, kama vile gharama ya maudhui au iwapo tunaweza kuchuma mapato kutoka kwake, kunaweza kuathiri mapendekezo yetu. Kwa mfano, Discovery Mode huwapa wasanii na kampuni za muziki fursa ya kubainisha nyimbo ambazo ni kipaumbele kwao, na mfumo wetu utaongeza ishara hiyo kwenye algoriti ili kubaini maudhui ya vipindi vya usikilizaji vilivyowekewa mapendeleo. Msanii au kampuni ya muziki inapowasha kipengele cha Discovery Mode kwenye wimbo, Spotify hutoza asilimia ya faida kwenye mitiririko ya wimbo huo katika maeneo ya mfumo ambapo kipengele cha Discovery Mode kinatumika (Kipengele cha Discovery Mode hakitumiki katika orodha zetu za kucheza za waratibu). Ishara hii huongeza uwezekano wa nyimbo zilizochaguliwa kupendekezwa, lakini si hakikisho la hilo kutokea. Tunapendekeza nyimbo ambapo kuna uwezekano wa juu kuwa wasikilizaji watazifurahia. Kama ilivyo kwa mapendekezo yote, tunazingatia msikilizaji asiposikiliza wimbo — ikiwa ni pamoja na zile zilizo katika kipengele cha Discovery Mode — na kuzingatia hili wakati tunabaini maudhui ya kupendekeza katika siku zijazo.