Sera ya Mali ya Uvumbuzi ya Spotify

1. Kuhusu Sera Hii

Sera hii ya Mali ya Uvumbuzi inaeleza jinsi tunavyoshughulikia madai ya ukiukaji wa haki za mali ya uvumbuzi kwenye tovuti, programu na huduma za Spotify ("Huduma za Spotify").

Spotify inaheshimu haki za mali ya uvumbuzi na inatarajia watumiaji wake waziheshimu pia. Katika matumizi ya Huduma za Spotify, watumiaji lazima watii Mwongozo wa Watumiaji wa Spotify, pamoja na sheria, kanuni na masharti yanayotumika na kuheshimu haki za mali ya uvumbuzi, sera na haki nyingine za watu wengine.

2. Hakimiliki

Hakimiliki ni nini

Hakimiliki ni haki ya kisheria inayolenga kulinda kazi halisi ya watayarishi (k.m., muziki, kazi ya sanaa, vitabu). Mmiliki wa hakimiliki ana haki ya kipekee ya kutumia kazi ya uvumbuzi kwa njia fulani ikiwa ni pamoja na kunakili, kusambaza na kuonyesha kazi hiyo. Kwa ujumla, hakimiliki hulinda kazi halisi; hailindi maelezo na mawazo. Hakimiliki pia kwa ujumla hailindi vitu kama vile majina, vichwa na wito; hata hivyo, haki nyingine ya kisheria inayojulikana kama haki ya chapa ya biashara inaweza kutumika (angalia hapa chini).

Kuna hali maalum za hakimiliki. Kwa mfano, katika nchi fulani, mtu asiye mmiliki wa haki anaweza kuruhusiwa kutumia hakimiliki ya mwingine ikiwa matumizi hayo ni ya haki, kama vile kwa madhumuni ya ukaguzi, ukosoaji au uigaji wa kubeza.

Jinsi ya kuripoti madai ya ukiukaji wa haki za hakimiliki

Ikiwa wewe ni mmiliki wa hakimiliki au ajenti wake, na unaamini kwamba maudhui yoyote yanayopatikana kupitia Huduma za Spotify yanakiuka kazi yako inayolindwa na hakimiliki, tafadhali tumia fomu hii ya wavuti kuwasilisha ripoti ya madai ya ukiukaji wa haki za hakimiliki. Au, unaweza kuwasilisha ripoti ya madai ya ukiukaji wa haki za hakimiliki kwa ajenti wa hakimiliki aliyetengwa wa Spotify kwa anwani ifuatayo, na maelezo yafuatayo:

  1. Utambulisho mahususi wa kila kazi inayolindwa na hakimiliki inayodaiwa kukiukwa;
  1. Maelezo ya mahali ambapo maudhui yanayoaminika kukiuka haki za hakimiliki yanapatikana kwenye Huduma ya Spotify au Tovuti za Spotify (tafadhali eleza kwa kina kadri uwezavyo na utoe URL ya kutusaidia kupata maudhui unayoripoti);
  1. Maelezo ya mawasiliano ya mlalamikaji, kama vile jina kamili, anwani, nambari ya simu na anwani ya barua pepe;
  1. Taarifa kwamba mlalamikaji ana nia nzuri ya kuamini kwamba matumizi ya kazi hiyo kwa namna inayolalamikiwa hayaidhinishwi na mmiliki wa hakimiliki, ajenti wake au sheria (kama vile sheria ya matumizi ya haki); na
  1. Taarifa kwamba maelezo yaliyo kwenye ripoti hiyo ni sahihi, na chini ya adhabu ya kusema uongo, mlalamikaji ni mmiliki wa haki ambayo inadaiwa kukiukwa, au ajenti wa mmiliki.
  1. Saini halisi au ya kielektroniki ya mmiliki (au mtu aliyeidhinishwa kumwakilisha mmiliki) wa hakimiliki inayodaiwa kukiukwa; na
  1. Taarifa kuwa unaelewa kwamba maelezo yako ya mawasiliano na/au ripoti yako itawasilishwa kwa mhusika anayedaiwa kutekeleza kosa la ukiukaji, na kuhifadhiwa kwa muda unaohitajika kwa madhumuni ya kisheria.

Bila maelezo ya hapo juu, huenda tusiwe na maelezo ya kutosha ili kushughulikia dai lako.

Unaweza kuwasiliana na ajenti wa Spotify wa hakimiliki aliyetengwa ifuatavyo:

Spotify USA Inc.

Kwa: Legal Department, Copyright Agent

4 World Trade Center, 150 Greenwich Street, 62nd Floor, NewYork, NY 10007

infringement-claim@spotify.com

Unapowasilisha dai ya ukiukaji wa haki za hakimiliki, Spotify inaweza kushiriki jina na anwani yako ya barua pepe kwa wahusika wanaodaiwa kutekeleza kosa la ukiukaji wa haki za hakimiliki, na kuhifadhi maelezo yako kwa muda unaohitajika kwa madhumuni ya kisheria. Tafadhali kumbuka, ripoti za ulaghai au matumizi mengine mabaya ya utaratibu huu yanaweza kusababisha kufungwa kwa akaunti yako na/au kuchukuliwa hatua za kisheria. Unaweza kutafuta ushauri wa wakili kabla ya kuwasilisha dai lako.

Spotify pia ina sera ya kufunga akaunti za wanaotekeleza makosa ya ukiukaji mara kwa mara, katika hali zinazofaa.

3. Chapa ya Biashara

Chapa ya biashara ni nini

Chapa ya biashara ni neno, wito, ishara au picha (k.m., jina la chapa, nembo) inayotofautisha bidhaa au huduma za mtu, kikundi au kampuni mahususi. Kwa ujumla, sheria ya chapa ya biashara inalenga kuzuia watumiaji kuchanganyikiwa kuhusu anayetoa au anayehusishwa na bidhaa au huduma mahususi.

Jinsi ya kuripoti madai ya ukiukaji wa haki za chapa ya biashara

Ikiwa wewe ni mmiliki wa chapa ya biashara au ajenti wake na unaamini kwamba maudhui yanayopatikana kwenye Huduma za Spotify yanakiuka haki zako za chapa ya biashara, tafadhali tumia fomu hii ya wavuti kuwasilisha ripoti ya madai ya ukiukaji wa haki za chapa ya biashara. Spotify inaweza kushiriki jina na anwani yako ya barua pepe kwa mhusika anayedaiwa kutekeleza kosa la ukiukaji na kuhifadhi maelezo yako kwa muda unaohitaji kwa madhumuni ya kisheria. Spotify pia ina sera ya kufunga akaunti za wanaotekeleza makosa ya ukiukaji mara kwa mara, katika hali zinazofaa.

4. Jinsi Tunavyoshughulikia Madai

Spotify hukagua madai yanayowasilishwa kupitia njia iliyobainishwa hapo juu. Tunapopokea dai, tutalikagua na kuchukua hatua inayofaa, ambayo inaweza kujumuisha kuondoa maudhui yaliyoripotiwa au kuzuia yasifikiwe katika nchi mahususi. Tunaweza kuwasiliana na mlalamikaji na mtumiaji au mtayarishi aliyetoa maudhui hayo kuhusu hatua tunayochukua/tunazochukua, ikiwa tutaamua kutochukua hatua yoyote, au ikiwa tunahitaji maelezo zaidi ili kutathmini dai hilo.

Maudhui yoyote yanayokiuka haki za hakimiliki au za chapa ya biashara yanaweza kuondolewa. Spotify pia ina sera ya wanaotekeleza makosa ya ukiukaji mara kwa mara, kumaanisha kwamba akaunti ya mtumiaji au mtayarishi anayewajibika kwa kutekeleza makosa mengi ya ukiukaji inaweza kufungwa. Ikiwa maudhui yatarejeshwa baada ya kukata rufaa au kwa sababu mmiliki wa haki anaondoa dai alilowasilisha, sera yetu ya wanaotekeleza makosa ya ukiukaji mara kwa mara itabainisha hivyo ipasavyo.

Ikiwa unaamini maudhui au akaunti yako imechukuliwa hatua kimakosa, au ikiwa ungependa kuomba ukaguzi mwingine wa uamuzi wa Spotify kuhusu dai lako, unaweza kupata fursa ya kukata rufaa. Maagizo kuhusu jinsi ya kukata rufaa yanapatikana kwenye mawasiliano ya barua pepe tutakayokutumia kuhusu dai husika.

Zaidi ya ripoti kutoka kwa watumiaji na wamiliki wa haki, tunatumia mseto wa ishara halisi na za kiotomatiki kugundua na kuondoa maudhui yanayoweza kukiuka haki za mali ya uvumbuzi za mwingine. Tunaendelea kuboresha juhudi zetu za kulinda mali ya uvumbuzi ya watayarishi.